TANZANIA: Maswali yaibuka kwa kusimamishwa kazi yule aliemtumia JK sms
Moshi. Nani alivujisha siri? Hili ndilo swali linaloumiza vichwa vya wananchi wengi sasa, baada ya Hospitali ya KCMC kumsimamisha kazi mtumishi wake, kwa madai ya kutuma ujumbe wa simu ya mkononi (sms) kwa Rais Jakaya Kikwete.
Mtumishi huyo, Paul Mhumba aliyekuwa Idara ya Uhasibu, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (Tughe), aliandikiwa barua ya kusimamishwa kazi Mei 5, mwaka huu.
Hatua hiyo imeibua sintofahamu kutoka kwa watu wa kada mbalimbali wakihoji imekuwaje ujumbe huo wa siri uliotumwa kwa Rais uliifikia taasisi iliyotajwa pamoja na namba ya mtumaji.
Wananchi mbalimbali waliopiga simu jana na wengine kuchangia kupitia mitandao ya kijamii, walidai mchawi wa mtafaruku huyo ni mtu aliyepewa ujumbe huo na Rais Kikwete ili aufanyie kazi.
Uongozi wa KCMC umekuwa mzito kutoa ufafanuzi wa suala hilo. Hata Kaimu Mkurugenzi wake mtendaji, Profesa Raymos Olomi alipopigiwa simu na kutumiwa ujumbe wa simu jana hakuweza kujibu.
Jana gazeti hili lililazimika kupeleka maswali kwake kwa maandishi kuhusiana na suala hilo ili kupata ufafanuzi wa nani aliyewapa taarifa ya kuwapo kwa ujumbe huo kwa Rais.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama jana alisema ameitisha kikao cha wataalamu wake leo ili kujadili suala hilo. “Nimepata simu nyingi zilizokuwa zikihoji suala hilo, nitakutana na wataalamu wangu kesho (leo) tuone nini hasa kimetokea maana hata mimi sijui kwa undani kiini hasa cha jambo hilo,” alisema Gama.
Wakati Gama akitoa kauli hiyo, uongozi wa KCMC umemtaka mtumishi huyo kupeleka ushahidi wake katika kikao cha mwisho cha kamati ya nidhamu kitakachokutana Mei 26, kujadili suala hilo.
Mhumba anataka Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Donan Mmbando awe shahidi wake kwa kuwa uongozi wa KCMC unadai ndiye aliyewapa ujumbe huo na namba ya mtumaji.
Katika barua yake kama mwenyekiti wa Tughe tawi la KCMC ya Mei 16, Mhumba alimwandikia barua Dk Mmbando akimwomba afike kutoa ushahidi.
Mhumba katika barua hiyo yenye kumb TUGHE/KCMC/05-4/2015, anadai Mei 4 na 5, katika kanisa dogo la Hagai KCMC, waumini walisomewa ujumbe uliodaiwa kutoka kwa Dk Mmbando.
Mbali na kumwomba katibu mkuu huyo kufika kutoa ushahidi, pia ameiomba Ofisi ya Rais Ikulu kuingilia kati suala hilo kwani linahusu faragha ya Rais ambayo imeingiliwa.
Category:
0 comments