WANAJESHI WA IRAQ WASONGA MBELE DHIDI YA KUNDI LA IS MJINI RAMADI
Wanajeshi wa Iraq wamepiga hatua kwenye zoezi lao dhidi ya wapiganaji wa Islamic State mjini Ramadi.
Wanajeshi hao ambao wanasaidiana na wapiganaji wa Kisuni wamo mita 500 kutoka afisi kuu ya baraza la mji.
Wamefanikiwa kukomboa mitaa kadha ya mji tangu kuanza kwa operesheni hiyo siku tano zilizopita.
Mji huo wenye Wasuni wengi umo kilomita 90 magharibi mwa Baghdad na ulitekwa na wapiganaji wa IS mwezi Mei.
Kutekwa kwa mji huo kuliaibisha sana jeshi la Iraq.
Wakati wa kuzinduliwa kwa operesheni Jumanne, jeshi la Iraq lilisema lilitarajia wapiganaji takriban 300 walio mjini humo wafurushwe katika kipindi cha siku kadha.
Lakini sasa kuna wasiwasi kwamba huenda wapiganaji hao wanashikilia mateka raia.
Wapiganaji wa IS wamepokonywa miji mingi waliyokuwa wameiteka nchini Iraq, huku wakiendelea kukabiliwa vikali na wanajeshi wa Iraq na wapiganaji wa Kikurdi.
Category:
0 comments