.

.

MAWAZO YA MWANANCHI JUU YA BUNGE

ZePLAN | 05:18:00 | 0 comments




Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mhimili mmojawapo kati ya mihimili mitatu ya dola.

Japokuwa chombo hiki kimeundwa kuisimamia na kuishauri Serikali kwa niaba ya wananchi, lakini Watanzania tumeanza kushuhudia vioja kama si vichekesho katika mkutano wake wa 20 unaoendelea.

Nimefuatilia mjadala huu lakini ninachokiona ndani ya Bunge ni kampeni mpya ndani ya mhimili huo yenye kulenga Uchaguzi Mkuu  na siyo kujadili bajeti kwa masilahi ya Watanzania.

Wiki iliyopita, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliwasilisha hotuba ya makadirio ya ofisi yake na Tamisemi kwa mwaka 2015/15.

Kilichojitokeza, badala ya wabunge kuchangia hoja hii kwa masilahi ya Watanzania, wao wakageuza Bunge kuwa uwanja wa kampeni kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu, jambo ambalo ni la hatari.

Walijibizana ili kukasirishana ili mwingine naye aweze kujibu. Hilo halivutii hata kidogo. Kimsingi walitakiwa waichambue bajeti iliyopo mbele yao lakini wakahamisha mada na kuingiza kampeni.

Ibara ya 63 (2) ya Katiba yetu, inasema Bunge ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambacho kitakuwa na madaraka ya kuisimamia Serikali na vyombo vyake vya utekelezaji.

Mbali na hilo, lakini ibara ya 63(3(a), imewapa wabunge wajibu wa kumuuliza waziri swali lolote kuhusu mambo ya umma katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo yako katika wajibu wake.

Kwa hiyo ni wajibu wa Serikali kupitia Waziri au Naibu Mawaziri ama Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kujibu maswali na hoja zinazoibuliwa na wabunge kwa sababu wanalipwa mishahara.

Ibara ya 58 ya katiba yetu hiyo iko wazi kuwa Mawaziri na Naibu Mawaziri watashika madaraka yao kwa ridhaa ya Rais na watalipwa mshahara, posho na malipo mengineyo kwa mujibu wa sheria.Sasa kilichojitokeza katika mijadala ya hotuba hii ya Waziri Mkuu, ni wabunge kugeuka wasemaji wa Serikali badala ya kuisimamia na kuishauri Serikali kama Ibara ya 63(2) inavyoelekeza.

Kitendo hiki cha baadhi ya wabunge karibu wote kutoka chama tawala kugeuka ‘mawaziri’ na kujibu hoja za wabunge, hakika kinaondoa  ile dhana ya kuwapo kwa mihimili mitatu.

Kama mbunge anatumia  muda wake karibu wote wa dakika 10 wa kujadili bajeti kwa maslahi ya wapiga kura wake, lakini akajikita kujibu hoja za wabunge wenzake, hakika anavunja katiba
Tunaambiwa mwaka wa fedha uliopita wa 2014/15, Serikali ilipeleka katika halmashauri zetu siyo zaidi ya asilimia 20 kwa Tamisemi, lakini wabunge hawakusimamia vizuri kuhoji suala hili.

 Sote tunafahamu, halmashauri zetu ndizo zinatekeleza miradi ya moja kwa moja katika maeneo yetu yakiwamo ya vijijini lakini  hazikwenda kwa kiwango kinachotakiwa, tunapataje maendeleo?

Nimuombe Spika, Anne Makinda na naibu wake, Job Ndugai kutumia kanuni ili kulifanya Bunge liwajibike kujadili mambo ya msingi ya bajeti badala ya kuonyeshana ubabe wa vyama.

Kama baadhi ya wabunge wataendeleza kashfa, kukebehiana na kutambiana nani mshindi 2015 badala ya kuichambua bajeti, chombo hicho kinaweza kupoteza mwelekeo machoni mwa Watanzania.

Kuna mambo ya msingi na makubwa ambayo tunataka wabunge wetu waibane Serikali ikiwamo suala la kuongezeka kwa rushwa na ufisadi, kuporomoka kwa shilingi na kupanda kwa mfumuko wa bei.

Tunataka kutoka sasa na kuendelea, wabunge wetu wajadili namna Watanzania walivyopigika kimaisha, huku wageni ndiyo wakifaidi rasilimali zetu. Tunataka wajadili migomo isiyokwisha nchini.

Category:

About GalleryBloggerTemplates.com:
GalleryBloggerTemplates.com is Free Blogger Templates Gallery. We provide Blogger templates for free. You can find about tutorials, blogger hacks, SEO optimization, tips and tricks here!

0 comments