QATAR:YAPINGA MADAI YA AMNESTY
Serikali ya Qatar imepinga madai ya shirika linalopigania haki za kibinadamu lenye makao yake nchini Marekani, Amnesty International, iliyodai kuwa maelfu ya wafanyi kazi nchini humo wanaojenga viwanja vitakavyotumika katika mashindano ya kombe la dunia la mwaka wa 2022 wangali wanadhulumiwa.
Amnesty International ilikuwa imedai kuwa licha ya serikali hiyo kuahidi kuwalipa wafanyikazi mishahara yao kwa wakati unaofaa wengi bado hawapokei malipo yao kwa wakati unaostahili.Aidha Amnesty imelalamikia vikali mtindo wa Hawala ambao unamzuia mfanyikazi kuondoka nchini humo pasi na ruhusa ya muajiri wake.
Serikali ya Qatar inasema kuwa mabadiliko yake yanaendelea ikisema kuwa tayari mfumo wa kielektroniki ndio unaotumika kuwalipa wafanyikazi hatua inayohakikisha kuwa wafanyikazi wanalipwa kwa wakati unaofaa.
Qatar inashikilia hoja kuwa inawalipa wafanyikazi hao kiwango cha juu cha mshahara zaidi ya pesa wanazolipwa makwao.
Serikali hiyo imesema kuwa kwa pamoja wafanyikazi hao wametuma nyumbani zaidi ya dola bilioni 12 mwaka uliopita.
Amnesty wanasema Qatar imepiga hatua kidogo sana kutekeleza ahadi nyingi walizozitoa mwaka jana, kwani wafanyakazi bado wanahitaji ruhusa kutoka kwa waajiri wao ,kubadili ajira au kuondoka nchini humo,mabadiliko ya malipo kwa wafanyakazi yanafanyika taratibu mno wakati ni jambo la muhimu mno.
Shirika hilo limesema katika ripoti yake kuwa FIFA inawajibu wa kimsingi kuhakikisha kuwa wafanyikazi hawadhulumiwi.
Amnesty inasema kuwa FIFA inapaswa kuchukua jumu la kuishinikiza Qatar kuwatendea haki wafanyikazi.
Waziri wa leba wa Qatar, Abdullah al-Kulaifi, amesema kuwa nchi yake inapania kutumia michezo hiyo ya kombe la dunia kufanya asilimia 90% ya mabadiliko katika sekta ya leba.
Ripoti hiyo ya Amnesty inawadia wakati ambao wadhamini wakuu wa FIFA , kampuni ya Visa ikielezea kusikitishwa mno na hali mbaya ya maisha ya wafanyikazi.
Wadhamini wenza Coca-Cola nao wameonya kuwa hawaungi mkono ukiukwaji wa haki za kibinadamu.
Mwandishi wa habari wa BBC Mark Lobel alikamatwa alipokuwa akiripoti kuhusu visa vya ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya wafanyikazi wanaojenga viwanja vya michezo na muundo msingi kwa jumla.
Afisa wa Amnesty Mustafa Qadri anasema kuwa takriban wafanyikazi milioni moja u nusu wanaendeleza ndoto ya Qatar 2022 licha ya taifa hilo kukosa kufanya mabadiliko yaliyohitajika katika sekta ya leba
Category:
0 comments