Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imeridhishwa na
matumizi ya fedha kiasi cha shilingi Bilioni 141 zilizotolewa na
Serikali kugharamia mradi mkubwa wa ujenzi wa bomba la maji kutoka
Mtambo wa Ruvu Chini,wilayani Bagamoyo kwenda jijini Dar es salaam
kufuatia ujenzi wake kukamilika.

Akizungumza mara baada ya Kamati hiyo kutembelea maeneo mbalimbali ya
mradi huo ikiwemo mtambo wa Maji wa Ruvu Chini ulioko Bagamoyo mkoani
Pwani, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la
Hanan’g Mhe. Mary Nagu amesema kuwa kamati kamati yake  imeridhishwa
na ubora wa  kazi iliyofanyika chini ya Usimamizi wa Mamlaka ya Maji
Safi na Maji Taka Dar es salam ( DAWASA).

Amesema mradi huo wenye urefu wa kilometa 56  umekamilika na kueleza
kuwa itakua historia kwa wananchi   wa Dar es salaam waliounganishwa
na mtandao wa mabomba ya DAWASCO kukosa maji.

Amesema kama kamati wamejiridhisha kuwa kiasi cha maji kinachozalishwa
kwa siku lita milioni 270 kutoka mtambo wa Ruvu Chini ni kingi  na
kueleza kuwa kiwango hicho kitaongezwa kwenye uzalishaji wa awali.
“Sisi kama Kamati ya Bunge tumeridhishwa na kazi nzuri iliyofanyika,
tumeshuhudia wenyewe maji yanayozalishwa ni mengi tunaipongeza
Serikali kwa kusikia kilio cha muda mrefu cha wakazi wa jiji la Dar es
salaam” Amesema Mhe.Nagu.
 
Amesema kazi iliyopo sasa kwa Serikali na mamlaka zinazohusika ni
kuhakikisha kuwa inakabiliana na na changamoto ya usambazaji wa maji
hayo ili wakazi wengi zaidi wa jiji hilo wanaunganishwe na mtandao wa
mabomba ya DAWASCO.

Amewataka DAWASCO kuifanya kazi hiyo kwa kasi  pia kuangalia upya
gharama za usambazaji wa maji pia kuwaangalia upya mawakala waliowekwa
kusimamia usambazaji wa maji ili kuwadhibiti wale wasiowaaminifu ili
wananchi waweze kupata maji kwa bei nafuu na kuepuka kutumia maji
yasiyo salama ambayo yamekuwa chanzo cha milipuko ya magonjwa ikiwemo
kipindupindu.

Aidha,ametoa wito kwa wananchi kulinda na kutunza vyanzo vya maji ili
upatikanaji wa maji hayo uwe endelevu huku akitoa wito kwa Wizara
kulifanyika kazi suala la kuwapatia maji wananchi wote wanaoishi
kuzunguka miundombinu mikubwa ya maji kote nchini ili kuimarisha
ulinzi na usalama.

Kwa upande wake Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge
akizungumza mara baada ya kukamilika kwa ziara ya wabunge hao kwenye
mtambo wa Maji wa Ruvu Chini amesema kuwa kukamilika kwa mradi huo
kutalifanya jiji la Dar es salaam kupata maji.

Amesema katika kuchukua hatua za kukabiliana na uhaba wa maji Serikali
iliamua kufanya maboresho makubwa mifumo ya maji kwa kujenga mipya na
kurekebisha ile ya zamani ili kuendana na kasi ongezeko la uhitaji wa
maji.

Amesema kazi kubwa ambayo inaendelea sasa ni kuhakikisha usambazaji
katika maeneo yenye mitandao ya mabomba na ile ambayo haikuwa na
mitandao ya mabomba ili kuwapatia maji ya uhakika.

” Naishukuru kamati kwa kuja kutembelea mradi wetu wametupa changamoto
ya kuhakikisha maji yanafika kwa wananchi, sisi kama serikali tuna
mpango wa kuhakikisha tunaondoa mifumo yote chakavu katika jiji la Dar
es salaam kwa kuweka mipya na hii tunaendelea nayo kwa kasi”
Amesisitiza.

Amesema kazi ya kuweka miundombinu ya usambazaji maji  katika jiji la
Dar es salaam imeshaanza akifafanua kuwa Serikali imeingia mikataba na
wakandarasi kuhakikisha kuwa kazi hiyo inafanyika kwa viwango.
Aidha, amesema kuwa baadhi ya maeneo ya jiji ikiwemo eneo la Kimara
kazi inaendelea huku maeneo ya katikati ya jiji miundombinu yake ni
chakavu inaendelea kubadilishwa ili iweze kuhimili wingi na nguvu ya
maji inayosukumwa
Ametoa wito kwa wananchi na wenye viwanda kutumia maji hayo ili
kulinda afya za walaji kwa kuwa maji hayo ni salama na yamepita kwenye
vipimo vya ubora ili kuepuka kutumia maji yasiyo salama ambayo
yamekuwa chanzo cha magonjwa.

” Tumeshatoa maelekezo viwanda vyote vya Dar es salaam vihakikishe
kuwa vinatumia maji haya, sasa tuna maji ya kutosha, waje
tuwaunganishe na maji haya japo baadhi yao wamekuwa wakijiunganishia
maji kiholela na kutumia visima wanavyochimba ambavyo si salama”.
Kuhusu Serikali kuhakikisha ulinzi wa mtandao wa bomba hilo lenye
urefu wa Kilometa 56 amesema kuwa kazi hiyo inafanywa na DAWASCO
ikiwahusisha viongozi na wananchi ambao mradi unapita katika maeneo
yao.

” Ni kweli ulinzi wa bomba hili ni muhimu,DAWASA wanaendelea kutoa
elimu kwa wananchi katika maeneo linakopita bomba, pia tumeshaweka
matoleo kwa ajili ya kuhakikisha tunawafikishia huduma ya maji
wananchi wanaoishi kuzunguka bomba hili ili nao wawe sehemu ya walinzi
wa mradi wao” Amesema.

Mhe. Lwenge ameongeza kuwa Shirika la Maji Safi na Maji Taka Dar es
salaam (DAWASCO) litaweka mfumo wa ulinzi wa kieletroniki ili kulinda
bomba hilo, mfumo huo utakua unapima kiwango cha msukumo wa maji
yanayotoka Ruvu Chini kisha kutoa taarifa kwenye vituo
vitakavyoanzishwa endapo itatokea hitilafu ya miundombinu hiyo.

Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo ambao ni Wabunge wakizungumzia
kukamilika kwa mradi huo wamesema kuwa wameridhishwa na kazi kubwa
iliyofanywa na serikali na kwamba itaondoa kero ya maji katika jiji la
Dar es-slaam.

Mbunge wa jimbo la Itirima, Mhe. Njalu Silanga ambaye  ni mmoja wa
wajumbe wa Kamati hiyo ameeleza kuwa ameridhishwa na kazi nzuri
iliyofanywa na Serikali kwa kuwa mradi huo umejengwa katika viwango
vya hali ya juu na kuongeza kwamba wakazi wa Dar es salaam sasa
watarajie kupata maji Safi na Salama.

“Naipongeza sana Serikali kwa kufanikisha mradi huu,kweli  wamefanya
kazi kubwa sana, mimi na wabunge wenzangu tumeona na tumeridhishwa na
utendaji wa Serikali katika kuhakikisha jiji la Dar es salaam linapata
maji safi na salama”

Ameiomba Serikali kuweka msisitizo katika uimarishaji wa miundombinu
ili kuwezesha maji kufika kwa urahisi katika makazi ya watu.

Naye Mhe. Dkt.Sware Semesi, Mbunge wa viti maalum mkoa wa Dodoma
akiuzungumzia mradi huo amesema kuwa ameridhishwa na miundombinu imara
iliyojengwa na kuiomba serikali kusimamia usambazaji wa huduma hiyo
kwa wananchi.

” Mimi pamoja na wabunge wenzagu tumeshuhudia mradi huu ni
mkubwa,kilichobaki kwa mamlaka zinazohusika ni kujipanga na
kuhakikisha kunakuwa na mgawanyo mzuri wa maji haya,kufanyika kwa
Uhakiki na ukusanyanji wa ankara za wateja unaoendana na matumizi
halisi ya maji hayo ili huduma hii iwe endelevu” Amesema.
Aidha, ametoa wito kwa DAWASCO kusimamia kikamilifu usambazaji wa lita
milioni 270 zinazozalishwa kwa siku na mtambo wa Ruvu chini kwenda
matangi  ya maji yaliyoko Chuo Kikuu Ardhi

imageMeneja wa Mtambo wa Maji wa Ruvu Chini Mhandisi Emmanuel Makusa (katikati) akiwaongoza Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kutembelea Mtambo wa Maji wa Ruvu
 
Chini,wilayani Bagamoyo  kujionea maendeleo yaliyofikiwa kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa bomba lenye urefu wa Kilometa 56 linalotoka katika mtambo huo kwenda jijini Dar es salaam.

image_1Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakiangalia sehemu ya kukusanyia maji kutoka mto Ruvu kwenye Mtambo wa Ruvu Chini.

image_2Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakiangalia mitambo ya kuchujia maji kutoka mto Ruvu kwenye Mtambo wa maji wa Ruvu Chini.

image_3.Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ( katikati) na baadhi ya wajumbe wakimsikiliza kwa makini Meneja wa Mtambo wa Maji wa Ruvu Chini Mhandisi Emmanuel Makusa mara
baada ya kutembelea sehemu ya kuchujia maji na kuchanganyia dawa.
image_5Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakiangalia eneo lenye pampu za kusukumia maji kutoka mtambo wa Ruvu Chini  kwenda matangi ya maji yaliyoko Chuo Kikuu Ardhi jijini
Dar es salaam.
image_6
image_8Eneo la kukusanyia maji kutoka mto Ruvu kwenda kwenye mtambo wa kusafishia Maji

image_9 image_11Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukamilisha ziara ya kutembelea mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Chini, Bagamoyo mkoani Pwani.