.

.

UWANJA WA NDEGE WAKIGOMA WABORESHWA KATIKA HADHI YA KIMATAIFA

ZePLAN | 00:47:00 | 0 comments


Serikali imesema awamu ya pili ya Upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kigoma itaanza rasmi Julai mwaka huu.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema zabuni kwa ajili ya ujenzi zitatangazwa badae mwaka huu ili kuuwezesha Uwanja huo kuwa na hadhi ya kimataifa na kuchochea fursa za utalii katika ukanda wa Magharibi na Mwambao wa Ziwa Tanganyika.

Zaidi ya Shilingi Bilioni 40 kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB), zinatarajiwa kutumika hivyo kuwataka wananchi ambao eneo lao liko katika Uwanja huo kuondoka mara moja mara baada ya kulipwa fidia.

“Nia ya Serikali ni kuongeza njia ya kuruka na kutua ndege kutoka urefu wa mita 1800 sasa hadi mita 3100 na hivyo kuruhusu ndege kubwa aina ya Boeing 737 kutua katika uwanja huo”, amesema Prof. Mbarawa.

Makame Mbarawa
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kulia), akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga mkoani Kigoma Bw. Godlove Longole wakati alipokagua Uwanja wa Ndege mkoani hapo. Wa pili kulia ni Mbunge wa kigoma Mjini Mhe. Zitto Kabwe akifatilia.

Prof. Mbarawa amewataka wananchi wa Kigoma kutoa ushirikiano mkubwa kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na Mamlaka ya Usafiri wa Anga ili zoezi la ujenzi lifanikiwe kwa haraka na kuepuka vikwazo vinavyoweza kuchelewesha mradi huo.

Naye Mbunge wa Kigoma Mjini, Mhe. Zitto Kabwe amewataka wananchi wa Kigoma na wawekezaji kujipanga kutumia fursa ya uwanja huo kuwekeza ili kukuza sekta ya utalii na usafirishaji katika Mwambao wa Ziwa Tanganyika pindi uwanja huo utakapokamilika.

“Tuna bahati kupata Serikali inayowekeza katika mkoa wa Kigoma, nawaomba wana Kigoma wenzangu tuepuke migogoro na kutumia fursa hii kuwekeza kikamilifu ili kukuza utalii katika ukanda wa Magharibi na kuongeza mapato katika mkoa wa Kigoma”, amesisitiza Mhe. Zitto.

Amemhakikishia Profesa Mbarawa kuwa Uwanja wa Ndege wa Kigoma utafungua usafiri wa Anga kwa ukanda wa magharibi na nchi jirani na hivyo kuongeza idadi ya watalii na watumiaji wa usafiri wa anga katika mwambao wa Ziwa Tanganyika,  hifadhi za Taifa za Gombe na Mahale na mikoa ya kanda ya magharibi.

Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Mkoani Kigoma Bw. Godlove Longole ameiomba Serikali  kukamilisha Ujenzi wa uzio, Jengo la Abiria, Mnara wa kuongozea ndege na huduma za zimamoto katika uwanja huo ili kuuwezesha kufanya kazi zake kwa viwango vinavyotakiwa.

Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma Bw. Mohamedi Issa amemhakikishia Waziri kwamba atasimamia mchakato mzima wa mradi wa ujenzi kwa uadilifu, uaminifu ili thamani ya mradi huo ili uwiane na ubora wa kazi itakayofanywa na hivyo kuuwezesha uwanja huo kufikia kiwango cha Code 4C kinachowezesha ndege zenye ukubwa wa Boeing 737 kutua katika uwanja huo.

Category:

About GalleryBloggerTemplates.com:
GalleryBloggerTemplates.com is Free Blogger Templates Gallery. We provide Blogger templates for free. You can find about tutorials, blogger hacks, SEO optimization, tips and tricks here!

0 comments