TTCL YAJA NA NEMBO MPYA, YABORESHA HUDUMA ZAKE SASA NI MWENDO WA 4LTE
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewataka wafanyakazi wa Kampuni ya Simu ya (TTCL), kuwa wabunifu ili kuhimili ushindani wa soko katika sekta ya mawasiliano na hivyo kuiwezesha kampuni hiyo kupata faida.
Akizungumza wakati akizindua nembo mpya ya kampuni ya TTCL na huduma ya 4G LTE inayowezesha huduma ya mawasiliano ya sauti na data kwa haraka Prof. Mbarawa amesema huu ni wakati wa kubadili mtazamo na kufanya kazi kisasa ili kuvutia wananchi kutumia huduma za TTCL.
“TTCL lazima mubadilike ili muweze kuendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia na hivyo kumudu ushindani uliopo sasa katika sekta ya mawasiliano”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Amewataka TTCL kuhakikisha kituo mahiri cha kutunzia taarifa (Data Centre), kinaanza mapema mwezi Juni ili kuwezesha wadau wengi kunufaika na kituo hicho.
Prof. Mbarawa amesema Serikali inaunga mkono TTCL na imetenga masafa ya 800 MHZ ambayo yataiwezesha TTCL kushindana na makampuni mengine ya watoa huduma ya mawasiliano na kuwaunganisha wateja wengi kutumia huduma za mawasiliano na data.
“Uzinduzi wa nembo mpya ya TTCL na huduma ya masafa ya 4G LTE uendane na ubunifu kwa wafanyakazi ili muwavutie watumiaji wengi wa simu na hivyo kupata soko kubwa na kuifanya TTCL kuchangia kikamilifu pato la taifa”, amesisitiza Waziri Mbarawa.
Prof. Mbarawa amesema mawasiliano ni kiungo muhimu cha kufanikisha ukuaji wa sekta za kilimo, taasisi za fedha, uwekezaji, ujasiliamali na utendaji kazi wa Serikali na sekta binafsi hivyo ubunifu katika utendaji utaiwezesha TTCL mpya kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amewataka wananchi kuzingatia maelekezo wanayopatiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kuhusu namna ya kuzitambua simu na vifaa feki na hatua za kufuata ili ifikapo Juni 16 zoezi la kuzifunga simu feki litakapotekelezwa wasiathirike.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL Bi. Edwina Lupembe amesisitiza kwamba TTCL imejipanga kuboresha huduma za fedha ili kuwezesha watumiaji wengi wa kampuni hiyo kunufaika na huduma ya kutuma na kupokea fedha.
“Tumekamilisha mradi mkubwa wa kusimika mitambo ya GSM, UMTS na LTE ambayo itakuwa na uwezo wa kutoa huduma ya mawasiliano 2G, 3G na 4G”, amesema Bi. Lupembe
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL Dkt. Kamugisha Kazaura amemhakikishia Waziri Mbarawa kuwa mabadiliko ya muonekano wa TTCL yataendana na mtazamo mpya wa wafanyakazi wenye lengo la kuiwezesha kampuni hiyo kuwa ya kisasa hapa nchini.
Amesema TTCL imejipanga kuboresha simu za mezani, mkononi, na huduma za intaneti ya haraka ili iweze kupata wateja wengi na hivyo kuongeza mapato yake.
“Teknolojia ya 2G GSM, 3G UMTS na LTE imeongeza nguvu kwa kampuni yetu kuleta ushindani katika soko la mawasiliano na zitaendelea kuongeza ufanisi na ubunifu wa huduma zetu kwa bei nafuu”, amesisitiza Dkt. Kazaura.
Tayari huduma ya 4G LTE inapatikana katika maeneo mengi ya Ilala, Temeke na Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Category:
0 comments