NAMNA UKAWA WALIVYO VUNJA BUNGE
Dodoma. Wabunge wa upinzani
wanaounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) jana walianzisha
tafrani bungeni na kusababisha kikao
cha Bunge kuvunjika saa 5.18 asubuhi
baada ya kusimama na kupaza sauti
wakishinikiza Serikali itoe kauli juu ya
hatima ya uboreshaji wa Daftari la
Kudumu la Wapigakura na upigaji wa
Kura ya Maoni kupitisha Katiba
Inayopendekezwa.
Huku wakiwa wamesimama walikuwa
wanapiga kelele wakisema, ‘hatutaki
kuburuzwa’, ‘tumechoka kupelekeshwa’,
Watanzania wapo njia panda’ na
‘tunataka majibu,’ ‘Bunge lisitumiwe
kuilinda Serikali’, ‘Waziri Mkuu yupo
bungeni kwa nini asitoe kauli’ na
maneno mengine mengi bila mpangilio.
Wabunge hao wa vyama vya NCCR-
Mageuzi, Chadema na CUF, kwa umoja
wao walimtaka Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda kutoa majibu hayo muda huohuo,
kabla ya jioni kutoa hutuba na
kuahirisha mkutano huo wa 19 wa
Bunge.
Baadaye jana usiku katika hotuba yake
ya kuahirisha Bunge hadi Mei 12,
utakapoanza Mkutano wa 20, Waziri
Mkuu Pinda alisema Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) itatoa taarifa siku za
hivi karibuni kuhusu upigaji wa kura ya
maoni.
“Ni dhahiri muda uliobaki kuanzia sasa
ni mfupi lakini Tume ndiyo
itakayotujulisha ratiba kamili,” alisema.
Sakata lilivyoanza
Kelele hizo zilitokana na hoja za
wabunge wawili, Suleiman Jafo wa
Kisarawe na yule wa Ubungo, John
Mnyika waliotaka Bunge lisitishe
shughuli zake zote lijadili suala hilo kwa
kuwa ni muhimu na Taifa halielewi
hatima yake, wakati Bunge lilikuwa
linaahirishwa jana.
Spika wa Bunge, Anne Makinda alikataa
suala hilo kujadiliwa, akisema ni hoja
iliyowasilishwa katika mkutano uliopita,
akataka Bunge liendelee na shughuli
zake, lakini wabunge wa upinzani
walikataa kukaa na wakaendelea kupaza
sauti.
Hata alipobadili kauli akasema,
“nimesema kauli itatolewa, wabunge hao
walisisitiza itolewe papohapo. Hata
alipowataka waondoke ndani ya ukumbi
huo, wabunge hao ambao ni wachache
ukilinganisha na wale wa CCM,
walikataa, wakisema; “hatutoki hadi
kauli itolewe.”
Kelele za wabunge hao zilimfanya Spika
Makinda kutoa kauli kali, “Njooni
mwendeshe (kikao) nyinyi basi. Njooni
hapa mkae tena wote.”
Baada ya kuona kelele hizo zimedumu
kwa dakika tatu, Spika Makinda
alilazimika kusitisha shughuli za Bunge
hadi baadaye (jioni), bila kutaja muda
ambao Bunge lingerejea na kuwaacha
wabunge wakiwa wamesimama katika
makundi ndani ya ukumbi wakijadili
tukio hilo.
Jafo ndiye aliyeanza kuomba mwongozo
wa Spika akitaka chombo hicho cha
kutunga sheria kisitishe kujadili jambo
lolote lile, badala yake kijadili
mustakabali wa Katiba Mpya, akitaka
Serikali iwasilishe muswada wa sheria
kwenye mkutano wa 20 wa Bunge (wa
Bajeti) ili Katiba ya Mpito ipitishwe.
Jafo alitaka Katiba Inayopendekezwa
ipitishwe kwa mpito ili kuondoa
sintofahamu ya watu wanaotaka kuwapo
mgombea binafsi, kupinga matokeo ya
urais mahakamani, kuweka ukomo wa
Bunge na wabunge na kuwapo kwa
Tume huru ya uchaguzi.
Alisema mambo hayo manne ambayo
yamekuwa yakipigiwa kelele yamo
katika Katiba Inayopendekezwa, hivyo
ni vyema ikapitishwa kwa mpito ili
mambo hayo tu manne yatumike katika
Uchaguzi Mkuu.
Alisema wananchi wamejitokeza kwa
wingi kujiandikisha kwenye daftari la
kudumu la wapiga kura lakini kuna
changamoto za upungufu wa vitendea
kazi, zikiwamo mashine za kielektroniki
za Biometric Voters Registration (BVR).
Alisema kutokana na hali hiyo, ni
vigumu upigaji Kura ya Maoni ya Katiba
Inayopendekezwa kufanyika Aprili 30,
mwaka huu kama ilivyopangwa.
Alisema upigaji kura ya maoni lazima
utanguliwe na utoaji wa elimu kwa
mpigakura, jambo ambalo kwa muda
uliobaki ni vigumu kufanyika.
“Tutumie mkutano wa 20 tuhakikishe
Serikali inaleta muswada wa hati ya
dharura ili Bunge lipitishe katiba ya
mpito, kwa sababu Taifa sasa hivi lipo
katika hali tete kila mtu anasema lake.
Endapo tutafanya hivyo tutakuwa na
katiba ya mpito ya kati ya miezi sita
hadi 12, itaturuhusu kufanya uchaguzi
na baadaye watu watakwenda kwenye
Kura ya Maoni wakiwa wamepata elimu
ya kutosha juu ya Katiba
Inayopendekezwa.”
Alisema uamuzi huo utalinusuru Taifa
na si busara kuruhusu nchi kuingia
katika kura ya maoni huku kukiwa na
mvutano.
Baada ya kauli ya Jafo, Spika Makinda
alisema: “Ulichokizungumza wala siyo
utaratibu. Kwanza suala hilo litatolewa
ufafanuzi jioni wakati Waziri Mkuu
akiahirisha Bunge.”
Wakati Jafo akiomba mwongozo huo,
Halima Mdee (Kawe - Chadema), John
Mnyika (Ubungo - Chadema), Felix
Mkosamali (Muhambwe - NCCR), Moses
Machali (Kasulu Mjini - NCCR),
Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini -
Chadema) na Mbatia walisimama bila
kufuata utaratibu na kupaza sauti
wakipinga mwongozo huo.
“Hivi huyu katumwa au nini.
Anazungumza vitu gani humu ndani,”
alisema Mdee na kuungwa mkono na
Machali, huku wakitakiwa kukaa chini
na Makinda.
Baada ya kutulia kwa mvutano huo
uliodumu kwa takribani dakika nne,
Mnyika aliomba mwongozo wa Spika
kwa kutumia kanuni ya 47 (1) na
kusema: “ Mpaka sasa uandikishaji wa
wapigakura nchi nzima haujakamilika
hata katika mkoa mmoja tu wa Njombe.
Watanzania wapo katika sintofahamu
kuhusu ni lini wataandikishwa kwenye
Daftari la Kudumu la Wapigakura.”
Aliongeza, “Jambo hili ni la dharura
kwa sababu limeshatolewa hoja ya
dharura katika mkutano uliopita wa
Bunge, ukaagiza (Spika) kamati ya bunge
ilishughulikie, majibu yatolewe kwenye
mkutano huu wa Bunge. Leo hii (jana)
mkutano unakwenda kufungwa bila
majibu kutolewa.”
Mnyika alitaka shughuli zote za Bunge
kwa siku ya jana zisitishwe na majibu
juu ya masuala hayo mawili yapatikane.
“Nimeomba miongozo juu ya jambo hili
mara mbili na mara zote Serikali kupitia
kwa Waziri Mkuu umeipa maelekezo ya
kutoa majibu lakini inakwepa kutoa
majibu,” alisema.
Alisema kwa mazingira hayo, hakuna
sababu ya kuendelea na mjadala wowote
katika kikao hicho cha Bunge mpaka
majibu yapatikane, akisisitiza kuwa kwa
mujibu wa Ibara ya 63 (2) ya Katiba ya
nchi, kazi ya Bunge ni kuishauri
Serikali.
Huku akimnyooshea kidole Pinda
Mnyika alisema: “Waziri Mkuu (Pinda)
yupo hapa anaweza kutoa majibu na
tukajadili jambo hili.”
Baada ya Mnyika kuwasilisha mwongozo
wake, Makinda alisema: “Hoja ya
Mnyika inafanana na ile iliyotolewa na
Jafo. Tuendelee Katibu (akielekeza
kuendelea na ratiba za Bunge).”
Katibu wa Bunge alianza kusoma
miswada minne iliyokuwa ikisomwa
kwa mara ya kwanza, ikiwamo miwili
ya habari na hapo ndipo wabunge hao
wa upinzani waliposimama na kuanza
kupiga kelele.
Wakiwa wamesimama, wabunge hao
walianza kupaza sauti, akianza Machali
ambaye aliwasha kipaza sauti kuwa,
“Hoja hii haifanani kabisa na ile ya
(Jafo), ile ya kwanza inataka majibu
mkutano wa 20 na hoja hii ya pili
inataka majibu katika kikao hiki cha
leo”.
Majibizano
Mnyika: Hoja hii itolewe majibu na
Waziri Mkuu yupo hapa. Atoe majibu
Machali: Tunataka majibu, tumechoka
kuburuzwa.
Makinda: Anawaburuza nani,
nimewaambia kwamba swali lile
litajibiwa leo (jana) na Waziri Mkuu.
Waziri kivuli njoo usome hotuba ya
kambi ya upinzani.
Huku wabunge hao wakiwa bado
wamesimama, Spika alimwita waziri
kivuli wa Wizara ya Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, ili asome maoni
ya kambi hiyo juu ya Mswada wa Sheria
ya Miamala ya Kielektroni ya mwaka
2014 na ule wa Makosa ya Kimtandao
wa mwaka 2015.
Hata hivyo, msemaji huyo hakwenda
kusoma maoni yake na badala yake
wabunge hao waliendelea kusimama na
kushinikiza kutaka majibu kutoka kwa
waziri mkuu.
Baada ya kuona hali hiyo inaendelea,
Makinda aliahirisha kikao hicho na
kiliporejea saa 10 jioni, hoja hizo
hazikuendelea, badala yake miswada
iliendelea kujadiliwa. Habari
zilizopatikana zilieleza kuwa Kamati ya
Uongozi ilikutana na kukubaliana
majibu yatolewe katika hotuba ya
kuahirisha Bunge.
Nje ya ukumbi
Wakiwa nje ya Ukumbi wa Bunge,
Mbunge wa kuteuliwa (NCCR-Mageuzi),
James Mbatia na mwenzake wa Bariadi
Mashariki (UDP), John Cheyo walisema
wanachokitaka kwa Serikali ni kauli tu
juu ya suala hilo na si jambo jingine.
Tofauti na ilivyozoeleka kwamba
wangeitana na kukaa kikao cha Kambi
ya Upinzani, wabunge hao baada ya
kutoka bungeni kila mmoja aliondoka
zake, huku wakisikika wakiambiana,
“Tukutane baadaye bungeni.”
Baadaye, Katibu wa Bunge, Dk Thomas
Kashillilah alisema Bunge lingeendelea
saa 10 jioni, huku akitupa lawama kwa
upinzani kwamba walifanya makosa
kugomea kuendelea kwa kikao cha
Bunge, badala yake kama walikuwa na
hoja walitakiwa kuiwasilisha kwa Spika.
Category:
0 comments