MENDE NA UMUHIMU WAKE KWA BINADAMU
Mende huchukiwa sana na watu na
huhusishwa na uchafu na maradhi. Lakini wajua kwamba wadudu hawa wana
manufaa makubwa sana kwa binadamu?
Mjini Havana, nchini Cuba kuna
aina ya mende ambao hufugwa kama wanyama vipenzi na hata visa vyao
husimuliwa kwenye hadithi, anasimulia Mary Colwell.
Kwenye kisa kimoja, mende kwa jina Martina huwafanyisha mtihani wanaotaka kumchumbia kwa kuwaudhi kila wanapomtembelea.
"Mwaga
kahawa kwenye viatu vyao uone watalichukulia vipi hilo,” anapendekeza
nyanyake Martina. "Ni muhimu sana kujua mumeo mtarajiwa hufanya nini
anapokasirika – mtihani wa kahawa hufanikiwa.”
Kuna aina 4,500 ya mende, na ni aina nne pekee ambao huwa waharibifu.
Wengi hawaishi karibu na nyumba za watu na hutekeleza jukumu muhimu katika ikolojia kwa kula vitu vilivyokufa na vinavyooza.
Baadhi wana sifa nzuri na huishi pamoja na kusaidiana katika kutafuta
chakula na makazi. Wana uwezo wa kuishi katika mazingira magumu. Aina
moja kwa jina Eublaberus posticus wanaweza kuishi mwaka mmoja kwa kunywa
maji pekee.
Wale wazito zaidi, huwa na uzani wa gramu 35, na
urefu wa sentimeta 8 na huishi Australia. Wale wadogo zaidi huishi Ulaya
na Amerika Kaskazini na wana urefu wa sentimeta moja pekee.
Badala
ya kuwachukia, wanasayansi huwafurahia sana na kuwatumia kwa manufaa ya
binadamu. Mwaka 1999, mende walitumiwa na Prof Robert Full katika Chuo
Kikuu cha California, Berkley, kumpa wazo la kuunda roboti ya miguu sita
iliyosonga upesi na kwa urahisi.
Mende huwa thabiti sana, na wakianguka huwa wanainuka upesi na kwa urahisi kwa kutumia mabawa.
Miguu ya mende pia imekuwa ikitumiwa na wavumbuzi wanaotengeneza miguu bandia ya kutumiwa na binadamu.
Kuna
pia mende ambao wamekuwa wakiunganishwa na kompyuta ndogo inayowekwa
mgongoni na kuongozwa kufika maeneo ambayo mwanadamu hawezi kufika.
"Nilipoona hili mara ya kwanza, nilishangaa sana,”
mtafiti mkuu katika mradi huo unaoendeshwa katika Chuo Kikuu cha A&M
cha Texas, Hong Liang anasema.
Mende wanatumiwa pia katika
matibabu. Wanasayansi kwa miaka mingi wamekuwa wakishangazwa na uwezo wa
mende kukaa muda mrefu maeneo yenye sumu na uchafu bila kudhurika.
Wamegundua kwamba huwa wanatoa kemikali za kupigana na sumu.
Wanaweza
kusaidia katika kutengeneza dawa za kusaidia binadamu kukabiliana na
bakteria zinazohangaisha sana watu kwa mfano E. Coli na MRSA ambazo
zimekuwa hazisikii dawa.
Hii si mara ya kwanza mende kutumiwa kwa
sababu za kimatibabu. Mwanahabari Lafcadio Hearn karne ya 19 alipitia
maeneo ya kusini mwa Marekani na kuripoti jinsi watu wenye pepopunda
walivyokuwa wakipewa chai iliyotengenezwa kwa kutumia mende.
“Sijui
ni mende wangapi hutumiwa hadi upate kikombe cha chai, lakini wakazi wa
New Orleans wana imani sana na tiba hii,” aliandika.
Leo katika
hospitali Uchina, krimu inayotengenezwa kwa kutumia ungaunga wa mende
waliosiagwa hutumiwa kutibu vidonda vya moto na pia humezwa kutibu
vidonda vya tumbo.
Mende wanahitajika sana hivi kwamba Wang Fuming
aliamua kufungua biashara ya ufugaji mende eneo la Shandong, mashariki
mwa Uchina. Huwa anafuga mende 22 milioni kwa wakati mmoja. Anasema
tangu 2010, bei ya mende waliokaushwa imepanda mara kumi.
Mende pia huliwa Uchina!
Category:
0 comments