Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imetoa taarifa kuhusu uhalali wa filamu ya Mapenzi ya Mungu kama ni halali kumilikiwa na Elizabeth Michael ‘Lulu’ kufuatia kuwepo kwa maneno kuwa hakustahili kutwaa tuzo ya African Magic Views Choice Award (AMVCA) sababu filamu hiyo haikuwa na umiliki wake.

Katika taarifa hiyo imeeleza kuwa kuhusishwa kwa watu mbalimbali katika utengenezaji wa filamu hakuwezi kubadili uhalali wa filamu na kudhibitisha kuwa filamu hiyo inamilikiwa kihalali la Lulu.

“Ili filamu ikamilike inahusisha watu mbalimbali wanaoshirikishwa kukamilisha filamu kuanzia mtoa wazo ambaye wazo hilo huwekwa katika mswada na mtaalamu jambo ambalo haliondoshi umiliki wa filamu,

“Tunapenda kuufahamisha umma kuwa mmiliki halali wa Filamu ya Mapenzi ya Mungu ni Msanii Elizabeth Michael (Lulu) na ndiye aliyepata tuzo kwani ana haki zote za kupata tuzo hiyo kama mmiliki halali wa filamu hiyo,” ilieleza taarifa hiyo.

Aidha taarifa hiyo iliongeza kuwa filamu hiyo ilitengenezwa na kampuni ya Proin Promotion na ilisajiliwa kwa namba ya usajili CO831190.