MADUKA YATEKETEA KWA MOTO TANZANIA
Moto mkubwa umezuka na kuteketeza vibanda vya maduka zaidi ya 150 katika mji wa Kayanga wilaya ya Karagwe mkoa wa Kagera magharibi mwa Tanzania. Moto huo ambao ulianza Jumatatu majira ya sa 2:00 usiku umeteketeza mali na bidhaa za aina mbalimbali kama mchele, sukari, nguo, simu, pamoja na bidhaa zingine.
Wafanyabiashara wengi wanasema walikuwa na mikopo na wengi wao hawana bima ya mali zao. Jonasi Nyarugenda ni miongoni mwa wafanyabiashara hao: “Moto umeteketeza stoo zangu nne zenye bidhaa mbalimbali kama sukari, mchele, ngano na mafuta,: anasema Jonas na kuongeza, “kwakeli ukitathimini kwa haraka siyo chini ya milioni 45 zimepotea.” Amesema kwamba alikuwa hana bima katika mkopo wake wa milioni 20 kutoka katika benki.
Hasara hiyo kwa kiasi kikubwa imechangiwa na ukosefu wa vifaa vya kuzima moto. Wananchi wa Karagwe imewapasa kusubiri gari la Zimamoto kutoka Bukoba Mjini (magari ya uwanja wa ndege) ambako ni kilomita 120 kufika karagwe mjini. Hata hivyo magari hayo yalikuta maduka mengi yamekwishateketea.
Diwani wa kata ya Kanoni wilaya karagwe Sabi Rwazo amesema tukio hilo limewastua na ni tukio la kwanza la moto kuunguza soko wilayani humo. Anasema tatizo la ukosefu wa gari la zima moto linachangiwa na uhaba wa fedha. “Mara nyingi katika bajeti yetu imekuwa ikishindwa kununua gari.” Amesema Rwazo na kusema maombi yao yako serikali kuu.
Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Deodatus Kinwiro amesema kuwa Serikali ya wilaya yake itapata gari la zima moto hivi karibuni, “Bahati nzuri nilikuwa Dar es Salaam, nimekutana na kamishna mkuu wa zima moto ameniahidi kunipatia gari jipya,” amesema Kinwiro na kuongeza kuwa, “wakati wowote gari hilo litafika wilayani Karagwe.”
Hata hivyo baadhi ya wananchi wanasema hawakubaliani na kauli hiyo ya mkuu wa wilaya kwa sababu wamekuwa wakitozwa kiasi cha TZS 30,000 kwa mwezi ili kuchangia huduma za zimamoto wilayani hapo lakini wanashangaa kwa nini hawapati elimu ya kujikinga na majanga, na hakuna hata gari la dharura.
Mpaka sasa chanzo cha moto huo hakijajulikana lakini taarifa za awali zimeonesha kuwa kuna Mamalishe mwenye kibanda sokoni hapo aliacha jiko lake bila kuzima hivyo likashika nguo zilizokuwa katika kibanda hicho na kusababisha moto kusambaa ghafla.
Category:
0 comments