SHILINGI MILIONI 137.8 ZATOLEWA NA TASAF
Mpango
wa Kunusuru Kaya Masikini Tanzania (TASAF III) umetoa zaidi ya
shilingi Milioni 137.8 kwa kaya masikini 3627 katika vijiji 57 wilayani
Serengeti mkoani Mara.
Hayo
yamesemwa na Mratibu wa TASAF Wilaya ya Serengeti Bi Nancy Nzota
alipokuwa akiongea na wananchi wa kijiji cha Gesarya, Kata ya
Rung’abure kuhusu malipo ya kaya hizo kuwa yamefikia awamu ya tano.
Alisema malipo ya fedha hizo yameyotolewa katika kipindi cha utekelezaji wa mpango huo kwa mwezi Machi hadi Aprili 2016.
“Fedha
hizi mnazopewa ni mbegu na mnapaswa kuzitumia kukidhi mahitaji muhimu
yakiwemo ya elimu, afya na kuanzisha shughuli za uzalishaji” alisema Bi
Nancy.
Bi
Nancy aliongeza kuwa, watendaji wa vijiji wanatakiwa kubaini kaya
zinazotumia fedha hizo kinyume na matakwa ya mpango huo ambapo amewataka
watendaji watakaogunduliwa waondolewe katika uwakilishi wa kaya na
mchakato wa kubadili wasimamizi/wawakilishi wapya wa kaya zao ufanyike
kwa utaratibu maalumu.
Aliwaonya
wanufaika wa mpango huo kutokutumia fedha hizo kwa shughuli
zinazokinzana na mpango huo kwani kufanya hivyo hakutawatoa wananchi
katika hali ya umasikini.
Alisema
kuwa elimu hasa ya ujasiriamali ilishatolewa kwa wanufaika katika kila
kijiji juu ya kuanzisha shughuli za ufugaji, kilimo na biashara ndogo
ndogo.
Aliongeza
kuwa pia elimu hiyo huendelea kutolewa mara kwa kwa mara na wawezeshaji
wa mpango wa TASAF ambao hutoa elimu hiyo kwa wananchi katika kila
awamu ya malipo.
Mpango
huu ulizinduliwa mkoani Dodoma, Agosti 2012 na Rais mstaafu, Dk Jakaya
Kikwete, ambapo kwa Wilaya ya Serengeti malipo kwa kaya masikini
lilianza rasmi Julai 2015 na limeonesha kuanza kuzinufaisha kaya hizo.
Category:
0 comments