SUDAN KUSINI YAPATA UWANACHAMA WA JUMUIA YA AFRIKA MASHARIKI
Wakuu wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wameikubalia Sudan Kusini kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo ya kikanda.
Mkutano
wa kilele wa Jumuiya hiyo jijini Arusha kaskazini mwa Tanzania
ulipitisha siku ya Jumatano (Machi 2) pendekezo la baraza la mawaziri
juu ya uwanachama wa Sudan Kusini na pia hali ya usalama nchini Burundi.
Kikao
hicho kilichodumu kwa muda wa takribani masaa matano kililikubalia taifa
hilo changa kabisa barani Afrika kuwa mwanachama wake wa sita, kuungana
na Tanzania, Rwanda, Burundi , Uganda na Kenya.
Rais wa
Tanzania ambaye ndiye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho, John Pombe
Magufuli, aliwaambia wajumbe wa mkutano huo wa kilele kwamba sasa "Sudan
ya Kusini ni mwanachama halali wa jumuiya" hiyo.
Mkutano
huo pia ulizungumzia kwa kina masuala ya maendeleo ndani ya jumuiya
ikiwemo mipango ya kujengwa kwa viwanda vya nguo na bidhaa za ngozi ili
kuondoa kabisa biashara ya uagizaji wa nguo kuukuu, maarufu kama
mitumba, katika nchi hizo katika miaka michachache ijayo
Mkutano
huo pia ulishuhudia uzinduzi wa pasi ya kusafiria ya kielektroniki
itakayotumiwa katika eneo la Afrika Mashariki pamoja na mwongozo maalum
wa kimaaadili katika biashara kwenye nchi wanachama wa jumiya hiyo.
Akizungumzia
kuhusu maendeleo ya jumuiya hiyo, Katibu Mkuu anayemaliza muda wake,
Dk. Richard Sezibera, amesema kuwa jumiya hiyo inasonga mbele kwani
itifaki mbalimbali zimepitishwa kuanzia ushirikiano katika soko la
pamoja, ushuru wa forodha na sasa wanaelekea kufikia hatua ya Afrika
Mashariki kuwa na sarafu moja itakayotumika katika nchi zote wanachama.
Amesema
kuwa tayari jitihada zinaendelea katika kuondoa vikwazo mbalimbali
katika sekta za mawasiliano, biashara na usafiri "ili kuwapa wananchi wa
Afrika Mashariki fursa ya kuufurahia na kufaidi muungano" huo.
Katika
mkutano huo, Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi hakuhudhuria na badala
yake alimtuma makamu wake wa pili, Joseph Butore, huku serikali ya Sudan
Kusini ikiwakilishwa pia na makamu wa pili wa rais, James Waniiga.
Category: