UMOJA WA KLABU YA WAANDISHI WA HABARI WATOA TAMKO JUU YA UTEKWAJI WA MUANDISHI SALMA SAID
Umoja
wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) umetoa tamko kuhusu
kutekwa kwa mwandishi wa habari wa Sauti ya Ujerumani Zanzibar (DW),
Salma Said ambaye ametoweka baada ya kutekwa na watu ambao
hawajafahamika jijini Dar es salaam, hali ambayo imeleta fadhaa na
mshtuko kwa waandishi, jamii na familia yake hasa katika kipindi hiki
cha kuelekea uchaguzi wa marejeo Zanzibar.
Ifahamike
kuwa kazi ya mwandishi wa habari ni kutoa habari juu ya kila
kinachoendelea katika jamii , hivyo kama kuna dosari , dosari hiyo ni ya
jamii na sio ya anayeieleza dosari .
UTPC
inalaani na kupinga utekaji uliofanywa ambao sababu zake bado
hazijulikani, hivyo tunaitaka serikali kuhakikisha Salma Said
anatafutwa, kupatikana na anaachiwa huru mara moja kwa kuwa Serikali
ndio yenye jukumu la kulinda raia wake.
Kama
utekwaji wa Salma umefanywa kutokana na kazi yake ya uandishi habari
tunalaani vikali hatua hiyo, vitendo hivi havipaswi kuendelea katika
nchi inayoheshimu misingi haki na Demokrasia, Vitendo vya namna hii
vinadumaza na kufifisha uhuru wa habari .
Tunapinga
kwa nguvu zetu zote waandishi wa habari kukamatwa na vyombo vya dola
au makundi ya kihalifu kwa visingizio ama vya uchochezi au maslahi ya
taifa.
Waandishi tutaendelea kufanya kazi zetu bila kujali vitisho vya aina yoyote ile kutoka kwa mtu yoyote au Serikali.
Imetolewa na
DEOGRATIUS NSOKOLO
RAIS WA KLABU ZA WAANDISHI WA HABARI TANZANIA -UTPC.
Category:
0 comments