.

.

CHADEMA HAKUNA KULALA WALA KUSINZIA

ZePLAN | 14:44:00 | 0 comments

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema) jana kilizindua
mkakati wake wa ushindi “Hakuna
kulala, hakuna kula mpaka kieleweke”
katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba kwa
kufungua mafunzo yatakayoendeshwa
nchi nzima kwa viongozi wa vyama na
Serikali za Mitaa.
Katika mkakati huo, chama hicho
kimeigawa nchi katika kanda 10 za
utekelezaji huku kikijipanga kuimarisha
nguvu zaidi katika Jiji la Dar es Salaam
lenye idadi kubwa ya wapigakura.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe alisema wakati wa uzinduzi wa
mkakati huo kitaifa jijini hapa kuwa
watafundisha viongozi wote wa chama
hicho na watangaza nia, mbinu za
uongozi bora na namna ya kushinda.
Mbowe alisema mpango huo wa
mafunzo ni sehemu ya utekelezaji wa
maazimio ya chama kwa kuwa
hawawezi kushika Serikali Kuu na
Serikali za Mitaa bila kuwa na viongozi
bora na weledi.
Alisema Chadema kitakwenda katika
kanda zote, majimbo ya kichama 242,
kata 4,852, matawi 22, 749, misingi
64,803 na kuwafikia viongozi 224,287 na
timu zote za mafunzo zimeshatawanyika
nchi nzima.
“Tunawafundisha viongozi wetu walio
tayari ndani ya chama au Serikali za
Mitaa namna ya kutekeleza wajibu wao.
Lakini tunawaimarisha wanaokusudia
kugombea nafasi mbalimbali kuwa
wagombea wazuri zaidi, kuandaa
ajenda za chama na namna ya kukamata
madaraka kwa kuwa safari ya kushika
Dola 2015 haina kizuizi,” alisema
Mbowe huku akishangiliwa.
Kuahirisha uchaguzi
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na
mamia ya viongozi na watia nia wa
Kanda ya Pwani ya chama hicho, Mbowe
aliitaka Serikali kutojaribu kabisa
kuahirisha Uchaguzi Mkuu kwa sababu
ya kusuasua kwa uandikishaji wa daftari
la kudumu la wapigakura kwa kutumia
teknolojia ya Biometric Voters
Registration (BVR) akitishia kuwa ‘moto
utawaka’.
Alisema Ukawa hawakusema chochote
wakati wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC) ilipoahirisha Kura ya Maoni ya
Katiba Inayopendekezwa kwa kuwa
ilikuwa batili na ilianzishwa kwa
masilahi ya Serikali na aliahirishwa na
wao wenyewe.
Aliitaka Serikali kuharakisha
uandikishaji wa daftari la kudumu la
wapigakura kwa kuwa imesalia miezi
mitatu na nusu kabla ya kuanza kwa
kampeni za Uchaguzi Mkuu hapo Agosti.
Alisema tarehe ya kupiga kura ambayo
ni Jumapili ya Oktoba ilifahamika tangu
awali kwa kuwa ni ya kikatiba lakini
mpaka sasa uandikishaji unasuasua
katika Mkoa wa Njombe wenye wapiga
kura 340,000 ambao alisema hawafiki
hata nusu ya waliopo Jimbo la Ubungo.
“Wanasubiri kama walivyofanya
kwenye kuahirisha Kura ya Maoni na ili
waseme ‘ndugu Watanzania kwa kuwa
tumechelewa kuandikisha wapigakura
tunaomba Bunge lako tukufu liongezee
muda kwa Serikali ya awamu ya nne’...
mtakubali?” aliwahoji wafuasi hao na
kujibiwa “Hapanaaaa”.
“Serikali ikijaribu tu kuahirisha
uchaguzi, nchi itawaka moto. Ikifika
tarehe 25 Oktoba, Rais Jakaya Kikwete
nenda Msoga (Bagamoyo) ukapumzike
utuachie Ukawa na nchi yetu.”
Kuimarisha ngome Dar
Katika kile ilichoita kuimarisha ngome
yenye kura nyingi, Chadema imetoa
maazimio matatu kwa viongozi na
wafuasi wake wa Dar es Salaam
kuhakikisha inashika nafasi zote za
uongozi hapo Oktoba.
Alisema jiji hili siyo tu makao makuu ya
Serikali, balozi za nchi mbalimbali, au
kitovu cha mapato, bali lina majimbo
saba ya kwanza kwa idadi kubwa ya
wapigakura kuliko mkoa wowote nchini,
hivyo kusiwe na utani katika kutekeleza
mikakati ya ushindi.
Mbowe, aliyesubiriwa kwa hamu tangu
saa tatu asubuhi na kufika saa 6.05,
alisema Jimbo la Ubungo ni la kwanza
na lina wapigakura wengi kuliko hata
mikoa ya Njombe na Katavi.
Akishirikiana na viongozi hao, Mbowe
aliweka maazimio kuwa, Ukawa
wanatakiwa kushinda majimbo yote,
nafasi zote za umeya na madiwani ili
kudhibiti mapato na kuleta maendeleo.
“Dhamana kubwa ya Taifa hili
inawategemea wana Dar es Salaam, kazi
tutakazozifanya kuanzia leo hadi siku ya
uchaguzi zitasaidia nchi hii kubadilika
au kuendelea kuwa na Serikali ya
mabavu ya CCM,” alisema.
Alia kuzuia mpasuko
Kuhusu ugawanaji madaraka ndani ya
Ukawa, Mbowe aliwataka makada hao
kuvumiliana na kuzishinda changamoto
zinazowakabili na kuwa Chadema na
viongozi wa umoja huo wanaendelea
vizuri na mipango ya ushindi.
Aliwaeleza wafuasi hao kuwa licha ya
watu kuwaombea mabaya, wao
hawatagombana zaidi ya kuungana
kuing’oa CCM.
Alisema wanaotangaza nia wapo wengi
kuliko nafasi zilizopo na atapatikana
mmoja katika kila nafasi na
watakaozipata, itakuwa kwa misingi ya
haki na siyo dhuluma.

“Wale wote watakaokosa nafasi za
kugombea ubunge na udiwani watambue
kuwa vita tunavyopigana Chadema na
Ukawa siyo ya kugombea madaraka.
Bado wana nafasi kubwa ya kulitumikia
Taifa hili kupitia Serikali yetu ya
ushirika,” alisema.
Huku akishangiliwa na kuonyesha
kujiamini, Mbowe aliongeza: “Tunahitaji
watendaji wa Serikali, ndiyo nyinyi…
msifikiri fursa ni ubunge pekee, zipo
nyingi lakini zipatikane kwenye misingi
ya haki, uwazi na kuheshimiana.”
Mbowe alibainisha kuwa CCM
hawatakiwi kugombana huku wakitegea
kusubiri mgombea wa Ukawa atangazwe
ili wamtangaze wa kwao, wakifanya
hivyo watasubiri sana na kwamba
mgombea wa ushirika wao atatoka muda
ukifika.
Ziara ya Dk Slaa
Akimkaribisha Mbowe, Naibu Katibu
Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema
Tanzania inahitaji viongozi makini
watakaoweza kukiondoa CCM
madarakani.
Huku akishangiliwa, Mnyika alisema
lengo kuu la chama hicho ni kushika
dola Oktoba mwaka huu, ndiyo maana
Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa yuko
Marekani kwa ajili ya kuzungumza na
Watanzania waishio huko na
kuimarisha uhusiano na mataifa rafiki
kwa kuwa Chadema kitashika dola.
Akizungumzia ziara hiyo, Mjumbe wa
Kamati Kuu ya Chadema, Mabere
Marando alisema Dk Slaa yuko
ughaibuni kuyafuta yaliyofanywa na
Serikali ya Rais Kikwete ili Ukawa iweze
kuwa na uhusiano mzuri na nchi za
kigeni.
Ongezeko la madiwani
Mnyika alisema kuongezeka kwa
madiwani wa upinzani katika mabaraza
ya madiwani na wabunge Dar es Salaam,
kumeonyesha ufanisi katika kusimamia
fedha za umma tofauti na hali iliyokuwa
kabla ya 2010.
“Baada ya kuongezeka kwa wabunge wa
upinzani katika Manispaa ya Kinondoni,
mapato ya ndani ya manispaa
yaliongezeka kutoka Sh7 bilioni mwaka
2010 mpaka Sh35 bilioni hivi sasa,”
alisema Mnyika ambaye anakaimu
nafasi ya Katibu Mkuu.
Mbunge huyo alisema ufanisi
unajitokeza kwa sababu viongozi wa
Chadema wanafanya kazi kubwa ya
kusimamia rasilimali za Taifa na
kuhakikisha haziibwi.
Alisema mabadiliko yameanza
kuonekana baada ya Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa wa mwaka jana ambao
Chadema ilishinda mitaa 93 iliyopo Dar
es Salaam kutoka mitatu kiliyoshinda
mwaka 2009.
“Lengo letu si kuongeza idadi ya
madiwani kwa ajili ya kuwa wapinzani,
bali kuwa na madiwani wengi katika
manispaa ya Kinondoni ili meya atoke
Ukawa kuiongoza halmashauri,” alisema
Mnyika huku wanachama
wakimshangilia.
Uimara wa Ukawa
Marando ambaye ni Makamu
Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani, alisema
Ukawa ni muungano ambao CCM haina
ubavu wa kupambana nao na kwamba
umedhamiria kukiondoa madarakani ili
kurudisha rasilimali za nchi kwa
wananchi.
Alisema wananchi wamechoshwa na
dhuluma za Serikali ya CCM na
kusisitiza kuwa Chadema kina viongozi
wengi makini na wazalendo ambao
watarejesha uhuru na haki kama
alivyopigania Mwalimu Julius Nyerere.
“Wananchi wamechoshwa na miaka 50
ya CCM madarakani na mwisho wao ni
Oktoba. Wanachotaka wananchi ni watu
wenye nyota ya uongozi, ndiyo maana
tumeanzisha mpango huu wa mafunzo,”
alisema Marando.
Mwalimu na ziara ya ushindi
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema -
Zanzibar, Salum Mwalimu alisema hiyo
ni awamu ya pili ya kutoa mafunzo
ambayo yatafanyika katika kanda za
Victoria na Nyanda za Juu Kusini na
Pwani na kubadilishana katika kanda
zilizosalia.
Alisema wameunda vikosi vitatu
vitakavyozunguka katika maeneo hayo.
Kikosi cha kwanza kitakwenda Kanda ya
Serengeti inayojumuisha mikoa ya Mara,
Shinyanga na Simiyu. Kikosi hicho
kitakachokuwa chini ya Mnyika
kitaendelea na mafunzo katika mikoa ya
Mwanza, Kagera na Geita.
Kikosi cha pili kitakuwa chini Mwalimu
mwenyewe na kitakwenda Kanda ya
Nyanda za Juu Kusini inayojumuisha
mikoa ya Mbeya, Rukwa, Njombe,
Iringa, Morogoro na kuhitimishwa Dar
es Salaam.
Mwalimu alisema kikosi cha tatu
kitaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa
Chadema – Tanzania Bara, Profesa
Abdallah Safari na kitatoa mafunzo
katika mikoa ya Pwani na Tanga.
“Kuanzia Jumamosi itakuwa ni hakuna
kulala, hakuna kula, mpaka kieleweke.
Ziara hii ya mafunzo itakuwa ni moto
nchi nzima,” alisema Mwalimu huku
wanachama wakipiga makofi.

Category:

About GalleryBloggerTemplates.com:
GalleryBloggerTemplates.com is Free Blogger Templates Gallery. We provide Blogger templates for free. You can find about tutorials, blogger hacks, SEO optimization, tips and tricks here!

0 comments