NAMNA YA KULIMA KITUNGU
Zao la vitunguu hulimwa karibu kila mahali hapa
nchini. Hata hivyo, mikoa inayolima kwa wingi ni
Tanga, Arusha, Iringa, Kilimanjaro, Singida,
Morogoro, Mara, Mbeya Dodoma na Manyara.
Zao hili ni la biashara na chakula. Ekari moja
inaweza kuzalisha gunia 80 – 100 za vitunguu
zikitunzwa kitaalam, na mkulima anaweza
kulima mara mbili kwa Mwaka kwa mbegu
kubwa ambazo huchukua hadi miezi mitano (5)
shambani. Bei ya wastani kwa gunia moja ni Tsh
60,000
MAMBO YA KUZINGATIA WA K ATI WA UZALISHAJI
Ili kupata vitunguu bora na vingi ni muhimu
kuzingatia kanuni za kilimo bora cha
vitunguu.Baadhi ya kanuni hizo ni kama
zifuatazo: -
1 - Kuchagua aina ya mbegu
• Chagua aina bora kulingana na matakwa ya
soko
• Pamoja na mahitaji ya soko ni muhimu pia
kuchagua aina inayovumilia magonjwa,
wadudu,kukomaa mapema na kutoa mazao
mengi na bora.
2 - Kuweka mbolea
Vitunguu hustawi vizuri kwenye udongo wenye
rutuba ya kutosha.
• Tumia mbolea za asili ili kurutubisha udongo
kwa lengo la kupata mazao mengi na bora.
• Iwapo ni lazima kutumia mbolea za viwandani
muone mtaalam wa kilimo ili akuelekeze namna
ya kutumia. Mbolea ikizidi huharibu ubora wa
vitunguu.
3 - Kumwagilia maji
• Kagua shamba kuona kama udongo una
unyevu wa kutosha. Iwapo unyevu ni mdogo
mwagilia maji kufuata mahitaji ya mmea.
Vitunguu vinapoanza kukomaa punguza
kumwagilia ili kuepuka kuoza
4 - Kupalilia
• Palilia mara kwa mara ili kudhibiti magugu na
kuwezesha vitunguu kutumia vizuri unyevu na
virutubishi vilivyoko kwenye udongo. Pia magugu
mengine huficha wadudu waharibifu kama vile
utitiri mwekundu.
• Wakati wa kupalilia epuka kukata mizizi ya
mimea.
• Pandishia udongo na kufunika shina la kitunguu
wakati wa kupalilia ili kuzuia jua lisiunguze
mizizi na kubabua vitunguu. Vitunguu
vilivyoungua na kubabuliwa ubora wake hushuka
napia huharibika upesi wakati wa kuhifadhi.
5 - Kudhibiti magonjwa na wadudu
Vitunguu hushambuliwa na magonjwa na
wadudu mbalimbali ambao huweza kusababisha
upungufu na ubora wa mazao. Ili kudhibiti tatizo
hilo kagua shamba mara kwa mara kuona dalili
za mashambulizi. Endapo kuna dalili za
mashambulizi, chukua tahadhari ya kunyunyuzia
dawa mapema kabla madhara hayajaleta
upotevu mkubwa.
6 - Kupanda kwa nafasi:
Zingatia nafasi ya kupanda inayopendekezwa ili
kupata vitunguu vyenye ukubwa uliokusudiwa.
Wastani ni inchi 4 - 5 kutoka kitunguu kimoja
hadi kingine, na inchi 12 - 18 kutoka mstari hadi
mstari na kipandwe inchi 1 - 1.5 chini ya udongo
MAANDALIZI KABLA YA KUVUNA
1 - Kukagua shamba
• Kagua shamba ili kuhakikisha kuwa vitunguu
vimekomaa. Vitunguu huwa tayari kuvunwa miezi
mitatu hadi mitano tangu kusia mbegu
kutegemea aina ya mbegu na hali ya hewa.Dalili
za vitunguu vilivyokomaa:
• Majani hunyauka na kuanza kukauka
• Asilimia kumi hadi 20 ya mimea huanguka
majani na shingo hulegea.
• Majani hubadilika rangi kuwa ya manjano na
baadaye kaki
2 - Kuvuna
Vitunguu vinapaswa kuvunwa mapema mara tu
vinapokomaa ili kupata mazao mengi na
bora.Uvunaji hufanyika kwa mikono ambapo
jembe uma hutumika kuchimbua au kulainisha
udongo.Udongo ukishalainishwa vitunguu
hung’olewa kwa mkono. Inashauriwa uvunaji
uanze asubuhi ili vitunguu viweze kunyauka na
kukomaza ngozi sehemu za michubuko. Vitunguu
visiwekwe juani na inapobidi kukomaza ngozi
shambani, majani ya vitunguu yatumike kufunika
vitunguu ndani ya matuta yake wakati wa
mchana ambapo kuna jua. Kusanya vitunguu
kwenye vikapu kisha vipeleke sehemu ya
kukaushia. Vitunguu vya kukaushia kwenye
kichanja ni bora zaidi, mizizi na majani
hupunguzwa na kuachwa urefu wa robo inchi .
Vitunguu vya kukausha kwa kunining’iniza
havikatwi majani bali hufungwa kwenye mafungu
na kupelekwa sehemu ya kukaushia.
Category:
0 comments